Serikali imesema kuanzia sasa, mtihani wa kidato cha pili utakuwa ni wa mchujo kuanzia
sasa, hivyo atakayefeli atatimuliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam jana,
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
alisema mtihani wa mwaka huu, matokeo yake yatatumika kama kigezo cha kuchuja
na kukariri kidato cha pili kwa watahiniwa watakaoshindwa kufikia wastani wa
ufaulu wa alama 30.
"Mtihani wa kidato cha pili kama ilivyo mitihani mingine
ya taifa ni muhimu sana. Matokeo ya mtihani huu hutumiwa na Baraza la Mitihani
la Tanzania (Necta) kama sehemu ya matokeo katika mtihani wa taifa wa elimu ya
sekondari kidato cha nne," alisema Dk Kawambwa.
Alisema mtahiniwa ataruhusiwa kukariri kidato cha pili mara
moja tu na endapo mtahiniwa atashindwa mtihani kwa mara ya pili kwa mwaka
utakaofuatia, itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi.
Dk Kawambwa alisema kurudishwa kwa mchujo katika mtihani huo ni
moja ya njiia ya kuboresha elimu nchini na kupata wanafunzi walio bora
nchini.
Alisema hayo ni mabadiliko ya kawaida na yataendelea kuwapo katika
sekta hiyo kila mwaka
.
"Tunachopambania hapa ni ubora wa elimu nchini na hii
itasaidia kuondoa wanafunzi wanaosemekana wanamaliza shule hawajui kusoma,
japokuwa mimi siamini kama ni kweli," alisema Dk Kawambwa.
Alisema mtihani huo utamalizika Novemba 16, mwaka huu na idadi
ya shule na vituo vilivyosajili watahiniwa mwaka huu ni 4,242 ikiwa ni ongezeko
la vituo 55 ikilinganishwa na vile vilivyosajiliwa mwaka 2011 ambavyo vilikuwa
4,187.
"Kwa hiyo kwa mwaka huu kuna ongezeko la asilimia 1.3,"
alisema Dk Kawambwa.
Alisema watahiniwa 442,925 wamejiandikisha kufanya mtihani.
Kati yao wasichana ni 214,325 (sawa na asilimia 48.39) na wavulana ni
228,600 (sawa na asilimia 51.61).
"Wizara inaagiza wadau wote wa elimu katika kanda,
manispaa na halmashauri za wilaya pamoja na wazazi kuhakikisha kuwa wanafunzi
wote walioandikishwa kufanya mtihani wanafanya bila kukosa," alisema Dk
Kawambwa.
Januari mwaka huu Serikali iliamua kurudisha mtihani huo kwa
lengo la kupunguza matokeo mabaya ya kidato cha nne.
Akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Philipo Mulugo, alisema kuwa uamuzi wa Serikali wa kurudisha mtihani huo,
umezingatia vigezo katika kuboresha matokeo ya kidato cha nne.
Mulugo alisema kuwa kuwapo kwa mtihani huo kutapunguza idadi ya
wanaoshindwa kufaulu kidato cha nne.
“Kumekuwa na wanafunzi wazembe ambao
wamefanya kupungua kwa idadi ya ufaulu kutokana na kukosekana kwa mtihani wa
kidato cha pili, ambao ndiyo mwongozo wa mwanafunzi kufanya vizuri katika
mitihani mbalimbali,” alisema Mulugo.
No comments:
Post a Comment