HASSAN MAAJAR TRUST NA RADAR EDUCATION WAKARABATI MAKTABA NA
KUTOA VITABU 900 KWA SHULE YA MAJIMATITU
Dar es Salaam, tarehe 17 Agosti, 2017: Hassan Maajar Trust kwa kifupi HMT , hivi karibuni iliadhimisha miaka sita ya juhudi za kuboresha mazingira ya Elimu nchini. Kwa kushirikiana na kampuni ya Radar Education imekarabati maktaba ya shule ya Msingi Majimatitu na kutoa vitabu zaidi ya 900. Hafla ya kukabidhi maktaba na vitabu ilifanyika katika shule ya msingi Majimatitu, Mbagala, wilaya ya Temeke, Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa HMT Balozi Bertha Semu-Somi na Meneja Mkuu wa Radar Education Bw. Arthur Walden, walikabidhi maktaba hiyo na vitabu kwa Mwalimu Mkuu, Bw. Abdallah Mgomi. Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Felix Lyaniva alikuwa Mgeni Rasmi.
Akiongea na Waandishi wa Habari jana, Balozi Semu-Somi alisema, " Hii ni mara ya tatu kwetu kuwa hapa Majimatitu. Mwezi Agosti 2015, HMT ilitoa msaada wa madawati thelathini (30), kwa ajili ya Kitengo cha watoto wenye ulemavu. Wakati wa kukabidhi madawati hayo, HMT ilishuhudia takribani asilimia 90% ya wanafunzi wakikaa sakafuni. Tuliazimia kuhamasisha uchangiaji kwa kuandaa matembezi ya hiari kwa ufadhili wa Bank M.
Kupitia matembezi hayo, HMT ilifanikiwa kuelimisha umma kuhusu uhaba wa madawati Majimatitu; wengi waliitikia wito na kusaidia. Aidha HMT ilitumia kiasi cha fedha kilichotokana na wakati wa matembezi kutengenezesha madawati 280 yenye kukaa wanafunzi watatu hadi wanne kila moja, na hivyo kunyanyua wanafunzi wapatao 850 kutoka sakafuni.
Katika kuchangia Elimu bora nchini HMT inalenga kuwajengea wanafunzi utamaduni wa kusoma vitabu. Mwaka huu, kwa kushirikiana na Radar Education, tumeamua kuiwezesha shule ya Majimatitu kwa kukarabati maktaba na tumetoa vitabu zaidi ya mia tisa.
Bwana Walden wa Radar Education alisema; “Kwa kushirikiana na HMT katika mradi huu wa Maktaba, kwetu imekuwa ni fursa nyingine ya kuchangia Elimu Bora Tanzania. Kwa leo tumetoa jumla ya vitabu 933. Ni matumaini yetu kuwa Wanafunzi watatumia vema msaada huu na kujijengea utamaduni wa kusoma vitabu.”
Miaka sita ya shughuli za HMT chini ya kauli mbiu ”Dawati kwa Kila Mtoto”, taasisi hii imefanikiwa kutoa madawati 9,000 ambayo yamenufaisha zaidi ya wanafunzi 30,000 katika mikoa 13 hapa nchini;. (Rukwa, Njombe, Singida, Mwanza, Pwani, Shinyanga, Kigoma, Lindi, Mbeya, Iringa, Mtwara, Dar es Salaam, na Kilimanjaro). “Tumepiga hatua kubwa katika ndoto ya kuhamasisha umma kuhusu adha wanayopata wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa chini na kuungana nasi kukabili adha hiyo. “aliongeza Balozi Semu-Somi.
No comments:
Post a Comment