Thursday, November 10, 2016

PRESS RELEASE - KISWAHILI



TAASISI YA HASSAN MAAJAR KUENDELEA
KUBORESHA MAZINGIRA YA ELIMU NCHINI

Taasisi ya Hassan Maajar (HMT) ambayo hivi karibuni ilitimiza miaka 5 imeendelea na juhudi zake za kuboresha mazingira ya elimu hapa nchini. Katika kipindi cha miaka mitano, taasisi hiyo imefanya kazi kwa kushirikiana na Bank M kama Mdhamini Mkuu hasa katika mradi wa HMT uitwao “Dawati kwa Kila Mtoto”.

Mwaka huu, Hassan Maajar Trust kwa kushirikiana na Bank M wanaandaa hafla ya kuchangisha fedha itakayofanyika tarehe 25 Novemba 2016 katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam. Mgeni rasmi katika hafla hiyo atakuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Kassim Majiliwa.

Akiongea na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchangishaji Fedha ya taasisi hiyo, Bw, Daniel Mwasandube alisema kuwa Hassan Maajar Trust wanafurahi  kushirikiana tena na Bank M na kuongeza kuwa ushirikiano wanaoupata kutoka Bank M tangu kuanzishwa kwa Taasisi yao mwaka 2011 umechangia kwa kiasi kikubwa sana kufanikisha miradi wanayoitekeleza. “Tumetimiza miaka mitano hivi karibuni, hadi sasa HMT imeweza kutoa madawati 9,000 ambayo yamenufaisha zaidi ya wanafunzi 30,000 katika mikoa 13 hapa nchini. Mikoa hiyo ni Rukwa, Njombe, Singida Mwanza, Pwani, Shinyanga, Kigoma, Lindi, Mbeya, Iringa, Mtwara, Dar es Salaam, and Kilimanjaro.

Taasisi yetu inatambua adha inayowakabili wanafunzi wanapojifunza kusoma na kuandika wakiwa wameketi sakafuni. Aidha HMT imefanikiwa kuhamasisha umma nchini Tanzania na kwingine kuunga mkono jitihada zetu katika kutatua tatizo la upungufu wa madawati nchini chini ya kauli mbiu; “Dawati kwa Kila Mtoto”. Tunawashukuru sana wadhamini wetu wote” alisema Mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa uamuzi wa Bank M kushirikiana na HMT umeonesha jinsi benki hiyo inavyojali kukuza maendeleo ya elimu hapa nchini. Serikali pia imeonesha kutambua jitihada hizi zinazofanywa na taasisi yetu kwa kushiriana na Bank M”, alisema Mwasandube.

Mwasandube pia alieleza kuwa kupitia fedha zitakazochangishwa kwenye hafla ya mwaka huu, HMT itaendelea na mradi wa madawati kwa kuwa upungufu wa madawati umeongezeka licha ya jitihada za Serikali kwa kuwa idadi ya wanafunzi nayo imeongezeka. Hata hivyo, HMT itaangalia zaidi samani na vifaa kwa ajili shule kwa Wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na Waalimu. Kubwa zaidi, HMT itawasha mshumaa kuangazia tatizo sugu la uhaba wa huduma ya vyoo  katika shule.

Kwa kuongezea, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Yusuph Sinare, alielezea jinsi walivyoridhishwa na hali ya uchangiaji kupitia kampeni mbalimbali zinazofanywa na HMT, na kwamba hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu, wamefanikiwa kuchangisha Shilingi za Kitanzania Bilioni 1.7 fedha taslimu na Shilingi za Kitanzania Milioni 140 ikiwa ni michango mali.

Hivi karibuni, Afisa Mtendaji Mkuu (Mtarajiwa) wa Bank M, Bi Jacqueline Woiso, alisema kuwa Benki yao inajivunia kushirikiana na Taasisi ya Hassan Maajar Trust katika mpango huu na aliipongeza taasisi hiyo kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa miaka 5 hadi sasa. “Kuwezesha wanafunzi zaidi ya 30,000 kukaa kwenye madawati ndani ya miaka 5 ni mafanikio ambayo tunayatambua na yanaashiria juhudi endelevu”.


No comments: